Chief Michael Lukumbuzya
Nilikuwa naitafuta picha ya hayati Chief Michael Lukumbuzya kwa miaka mingi bila mafanikio. Sababu ya kuitafuta picha ya Chief Lukumbuzya ni kisa alichonihadithia Bi. Mwamvua biti Masha mke wa marehemu Abdulwahid Sykes maarufu akijuikana kwa jina la mwanae wa kwanza Daisy hivyo tukimuita Mama Daisy.
Nilikuwa kila nikipata fursa ya kuwa na mama yangu Bi. Mwamvua, yaani Mama Daisy nikipenda kumdodosa mambo yalivyokuwa wakati wa ukoloni walipokuwa wanapambana na Muingereza, kwanza kichinichini katika miaka ya mwanzo ya 1950 wakati wa TAA kisha wakipambana na mkoloni dhahiri baada ya kuunda TANU mwaka wa 1954.
Bi. Mwamvua alikuwa wakati mwingine bila kutegemea akiniangushia habari muhimu kupita kiasi. Mfano siku aliponiambia kuwa nafasi ya president wa TANU nafasi ile ilikuwa ya Chief Kidaha Makwaia lakini alikataa ndipo bahati ikamuangukia Julius Nyerere.
Chief David Kidaha Makwaia
Iko siku akanieleza taharuki iliyotokea nyumbani kwa Abdul Sykes baada ya Nyerere kula chakuka kilichomfanya tumbo limkate na ikadhaniwa kuwa amelishwa sumu.
Mkasa huu ulitokea wakati mama yake Nyerere, Bi. Mugaya Nyangombe yuko na Mama Maria Nyerere vilevile wamekaa uani na akina mama wengine na Abdul Sykes, Nyerere na viongozi wengine wako nyumba kubwa wanapanga mipango ya kupeleka harakati mbele.
Mama yake Nyerere alianza kulia akiamini kabisa kuwa mwanae katiliwa sumu katika chakula. Mama Daisy alikuwa na habari nyingi sana za nyakati zile. Historia ya TANU kama zilivyo nyaraka na picha zake nyingi zimo mikononi mwa watu.
Mfano mwingine ni wa mkutano wa kwanza wa Wanawake wa TANU uliokuwa ukifanyika Arnautoglo Hall na yeye alikuwa yuko nyumbani anafanya shughuli zake. Anasema, ‘’Aliporudi nyumbani Bwana Abdul kanikuta nimekaa, akaniuliza wewe hukwenda mkutanoni? Wenzako wote wako Arnautoglo…’’ Bi. Mwamvua anasema hapo hapo akachukua baibui lake na kuelekea mkutanoni.
Wasemaji wakuu walikuwa Bi. Titi Mohamed na Bi. Tatu biti Mzee. Huu ndiyo mkutano wa kwanza wa wanawake wa TANU.
Kushoto Mama Daisy na mbele yake ni Bi. Titi Mohamed
na Bi. Zainab mke wa Tewa Said Tewa
Katika mazungumzo kama haya ndipo siku moja akanihadithia habari za Chief Luumbuzya. Anasema walitoka Dar es Salaam yeye mumewe kwenda Nansio, Ukerewe kumtembelea Hamza Mwapachu.
Anasema walipanda meli Mwanza pamoja na Chief Lukumbuzya kuelekea Nansio. Lukumbuzya alikuwa anatokea Makerere Uganda alipokuwa anasoma anarudi nyumbani likizo. Abdul Sykes na Michael Lukumbuzya hawakuwa wanajuana.
Hamza Mwapachu alikuwa amekusanya wananchi na kikundi cha ngoma kuja kumpokea bandarini Nansio President wa TAA Abdulwahid Sykes. Lukumbuzya alishangazwa kukuta sherehe bandarini akifanyiwa mtu ambae yeye hakuwa anamjua na akiuliza anaambiwa ni mgeni kutoka Dar es Salaam.
Lukumbuzya alipigwa na butwaa kuona mapokezi ya watu wake wa Ukerewe wakiwa katika nderemo wakati yeye chief hakuna hata mtu alikuwa anajua kuwa yumo katika meli ile ile. Baadae Hamza Mwapachu alimfahamisha yule mgeni waliokuja kumpokea pale alikuwa nani katika siasa za Tanganyika.
Simulizi kama hizi zilinifikirisha sana katika kutaka kuwajua wazalendo wa wakati ule. Hamza Mwapachu alikuwa anafanya haya ya kukusanya wananchi kumpokea kiongozi wa Waafrika chini ya pua za Waingereza bila kujali nini kitampata licha ya kuwa yeye kupewa uhamisho kupelekwa kisiwani Ukerewe peke yake ilikuwa ni adhabu, kwa hakika ni kifungo khasa cha kumtia kuzuizini asiweze kuenedeleza mipango yake ya kuunda chama cha siasa.
Uhuru ulipopatikana Chief Michael Lukumbuzya alipelekwa nje ambako alikuwa balozi na mwisho akawa balozi Canada ambako huko ndiko umauti ulikomfika.
Abdulwahid Sykes